+255 222215701   info@mloganzila.or.tzWatumishi Mloganzila watakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ya moto.

May 10 2022

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, wakati wa ufunguzi wa mafunzo yanadharia na vitendo yaliyotolewa kwa watumishi mbalimbali yenye lengo la kukabiliana na majanga ya moto.

 Baadhi ya watumishi waliohudhuria mafunzo hayo wakimsikiliza kwa makini mtoa mada. 

 Mkaguzi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Elinimo Shang’a akitoa elimu juu ya kinga na tahadhari za kuchukua dhidi ya majanga ya moto.

Mmoja wa watumishi akifanya zoezi la kuzima moto mara baada ya kupatiwa mafunzo ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto.

Mmoja wa watumishi akifanya zoezi la kuzima moto mara baada ya kupatiwa mafunzo ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto.

Watumishi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila wamepatiwa mafunzo ya namna mbalimbali za kujikinga na kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ya moto.

Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa njia ya nadharia na vitendo yamelenga kuwajengea uwezo watumishi namna ya  kukabiliana na majanga ya moto katika maeneo ya hospitali.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa  mafunzo hayo,   Naibu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi amesema lengo la kuandaa  mafunzo hayo ni kuwawezesha watumishi kufahamu  njia gani sahihi ambazo wanatakiwa kuchukua wawapo kazini au majumbani mwao endapo moto utatokea.

“Watumishi wengi hawajui hatua ambazo wanatakiwa kuchukua endapo moto utatokea; vilevile wengi wetu hatujui namna ambavyo tunaweza kuzuia majanga ya moto kutokea kwahiyo  nina imani mafunzo haya yatasaidia kukabiliana na majanga ya moto” amesema, Dkt. Magandi.

Naye Mkaguzi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Bw. Elinimo Shang’a, amesema kuwa watu wengi hawajui njia sahihi za kukabiliana  na majanga ya moto kutokana na kutokua na elimu juu ya aina za visababishi ambavyo vinaweza kupelekea moto kutokea .

“Watu wengi wanaathirika na majanga ya moto kwa kushindwa kukabiliana na moto hasa ukiwa kwenye hatua za awali na kuacha  usambae na kuteketeza vitu mbalimbali” amesema,  Bw. Shang’a.

Mafunzo hayo yameratibiwa na uongozi wa hospitali umehusisha zaidi ya watumishi 100 kutoka idara mbalimbali.