+255 222215701   info@mloganzila.or.tzWataalam watakiwa kutumia ujuzi waliopata kuisaidia jamii

Sep 14 2022

Naibu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili –Mloganzila Dkt. Julieth Magandi akifungua mafunzo ya kupima magonjwa ya moyo kwa kutumia kifaa maalum kiitwacho (echocardiography) yanayofanyika hospitalini hapo.Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya kutumia kifaa maalum cha kupima magonjwa ya moyo wakiwa kwenye mafunzo.Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya kutumia kifaa maalum cha kupima magonjwa ya moyo wakiwa kwenye mafunzo.Mkurugenzi wa mafunzo hayo kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), Dkt. Pilly Chillo akitoa maelezo ya utangulizi ya mafunzo hayo kabla ya ufunguzi.Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi akiwa na Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi.Viongozi wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo.Wataalamu wa afya kutoka ndani na nje ya nchi wanaojengewa uwezo wa namna ya kufanya vipimo na kutambua magonjwa ya moyo kwa kutumia kifaa maalumu kiitwacho Echocardiography wametakiwa kuwa mabalozi wazuri na kuitumia taaluma waliyoipata kwa kuisaidia jamii.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi wakati wa kufungua mafunzo maalum yanayolenga kuwajengea uwezo wataalamu wa afya namna ya kufanya vipimo vya moyo kwa kutumia kifaa maalum kiitwacho Echocardiography yaliyoratibiwa na Kituo Cha umahiri cha kufundisha na kufanya utafiti wa Magonjwa ya moyo (The East African Centre of Excellence in Cardiovascular Sciences).

Dr. Magandi ameongeza kuwa wataalamu wanapaswa kutumia ujuzi huo kusaidia jamii na pia amewapongeza wote walioshiriki mafunzo haya na kusema kuwa ujuzi watakaoupata ni mkubwa na muhimu sana hivyo wanapaswa kuitumia kama ilivyokusudiwa

“Mnatakiwa kujifunza kwa bidii ili ujuzi mtakaoupoata hapa uwawezeshe kuisaidia jamii kutambua magonjwa ya moyo na kupatiwa matibabu kwa wakati” amesema Dkt. Magandi.

Akitoa mada katika mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Prof. Mohamed Janabi ameeleza ukubwa wa matatizo ya magonjwa ya moyo hapa nchini, Afrika na duniani kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa mafunzo hayo kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), Dkt. Pilly Chillo amesema mafunzo hayo yamepata mwitikio mkubwa kutoka hospitali mbalimbali za ndani na nje ya nchi kwa kuleta wataalam wao kujifunza, ambapo baadhi yao wametokea nchi jirani za Kenya na Zambia.

Dkt. Chillo ameongeza kuwa mafunzo haya yatafanyika kwa wiki nne, kati ya hizi wiki mbili ni kwa njia ya nadharia  na wiki nyingine mbili  zitakuwa kwa vitendo. 

Zaidi ya watumishi 40 wanahudhuria mafunzo hayo yanayofanyika kwa ushirikiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Chuo Kikuu cha Afya na  Sayansi  Shirikishi Muhimbili  (MUHAS) na Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).