+255 222151367/9   info@mloganzila.or.tzMloganzila kuanzisha huduma ya upasuaji wa matundu madogo kwa kutumia video.

Jul 16 2021

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga&Mloganzila) Prof. Lawrence Museru akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya upasuaji wa matundu madogo (laparoscopic surgery) kwa kutumia video yaliyofanyika Mloganzila.

Baadhi ya washiriki wakifatilia  mafunzo ya upasuaji wa matundu madogo kwa kutumia video .

Daktari Bingwa wa upasuaji kutoka Arusha Medical Centre, Dkt. Paul Kisanga akitoa mada wakati wa mafunzo hayo.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Hospitali ya Muhimbili- Mloganzila Dkt. Julieth Magandi wakwanza kulia akifuatlia mafunzo ya upasuaji wa matundu madogo kwa kutumia video yanayoendeshwa hospitalini hapa.

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru akiwa pamoja na wakufunzi wa mafunzo ya upasauaji wa matundu madogo kwa kutumia video. Kulia ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi.

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga & Mloganzila) Prof. Lawrence Museru amesema hospitali itaendelea kuwajengea uwezo madaktari na wauguzi ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia yanayotokea katika sekta ya afya.
Prof. Museru ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku ya tatu yenye lengo la kuwajengea uwezo wataalam kufanya  upasuaji wa matundu madogo kwa kutumia video yaliyofanyika Muhimbili Mloganzila.
Prof. Museru amesema huduma ya upasuaji kwa kutumia matundu madogo inahitaji uwekezaji mkubwa wa wataalam, vifaa tiba na manufaa yake ni makubwa ukilinganisha na gharama.
“Nafurahi sana kufanyika kwa mafunzo haya katika kutoa huduma teknolojia haiepukiki na Muhimbili haiwezi kukwepa tunarajia baada ya mafunzo haya utendaji wetu  uwe tofauti na sasa” Aliongeza Prof. Museru.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt Julieth Magandi amesema baada ya mafunzo haya hospitali itaanza kutoa huduma za upasuaji wa matundu madogo kwa kutumia video.
Dkt. Magandi amesema huduma hizo zitaanza kutolewa wiki ijayo kwa kuanza na idara ya magonjwa ya akina mama na idara ya upasuaji wa jumla , ambapo kwa wakina mama upasuaji utafanyika kila ijumaa ya wiki na kwa idara ya upasuaji wa jumla itakuwa kila  jumanne ya wiki.
“Ninawakaribisha wananchi hospitali ya Mloganzila kuja kupata huduma hii, vifaa tunavyo na wataalam wanapatiwa mafunzo,hivyo kuanzia wiki ijayo huduma hii itaanza kutolewa rasmi”. Amesema Dkt. Magandi
Akizungumzia faida ya kutumia huduma hiyo Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC), Dkt. Paul Kisanga amesema huduma za upasuaji wa matundu madogo kwa kutumia video (laparoscopic surgery) itasaidia wagonjwa kukaa muda mfupi hospitalini, kupunguza maumivu na kuondoa uwezekano wa mgonjwa kuwa na makovu makubwa. 
Dkt. Kisanga amesema mafunzo haya yatasaidia washiriki kujifunza mbinu mpya za kufanya upasuaji na kubadilishana uzoefu wa namna ya kufanya upasuaji wa matundu madogo kwa kutumia video
Mafunzo haya yamehusisha wanafunzi wanaobobea katika magonjwa ya upasuaji,  madaktari bingwa wa upasuaji kutoka MNH-(Upanga na Mloganzila) ,Amana, Temeke,Mwananyamala na mwakilishi wa Pyramid ambao wamesaidia kufanikisha ujio wa baadhi ya wakufunzi, Wauguzi na wataalam wa usingizi.