LOADING...

+255 222151367/9   info@mloganzila.or.tzMloganzila yapatiwa msaada wa mashine ya uchunguzi wa macho

Feb 23 2021

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi (kushoto) akizungumza wakati wa kupokea msaada wa mashine ya kufanyia uchunguzi wa macho (Slit Lamp Biomicroscope), katikati ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho Muhimbili-Mloganzila Catherine akifuatiwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Vision Care Bw. Taegyun Kim

Dkt.Magandi pamoja na Bw. Kim wakisaini hati ya makubaliano ya kuimarisha na kupanua wigo wa kuzuia upofu na kuimarisha huduma za afya ya macho.

Dkt. Catherine Makunja akitumia mashine hiyo kumpima mgonjwa mwenye matatizo ya macho.

Pichani ni muonekano wa mashine iliyokabidhiwa leo katika Hospitali ya Mloganzila.

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imepokea msaada wa mashine ya  uchunguzi wa macho (Slit Lamp Biomicroscope) yenye thamani ya takribani TZS. 20Mil ambayo itatumika kufanya uchunguzi kwa watu wenye matatizo ya macho.

Msaada huu umetolewa na Taasisi ya Vision Care inayojihusisha mapambano dhidi ya matizo ya upofu duniani.

Akipokea Msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema mashine hiyo itasaidia utendaji kazi katika Idara ya Magonjwa ya Macho.

“Msaada huu umekuja wakati muafaka kwani mashine hii tunaihitaji hivyo uwepo wake utaongeza tija katika huduma zetu, tunawashukuru sana kwa kuendelea kuboresha sekta ya afya Mloganzila”amesema Dkt. Magandi.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho Muhimbili-Mloganzila Catherine Makunja amesema mashine ya Slit Lamp Biomicroscope ni muhimu kwani kila mgonjwa anayefika kupata huduma katika Kliniki ya Magonjwa ya Macho lazima apimwe kwa kutumia mashine hii.

“Mashine hii inasaidia kukuza jicho na kumuwezesha daktari kuona kinachoendelea ndani ya jicho kwakuwa jicho ni kiungo kidogo” amefafanua Dkt. Makunjna.

“Katika Kliniki ya Magonjwa ya Macho Mloganzila, kwa mwezi tunawaona wagonjwa 290 hadi 380 ambapo kila mgonjwa lazima apimwe na mashine hii” amesema Dkt. Makunja.

Kwa mujibu wa Dkt. Makunja tatizo la macho limeongezeka kwa sasa kutokana na madiliko ya mfumo wa maisha na watu wengi kutokuwa na uelewa mpana juu ya magonjwa hayo, matatizo makubwa zaidi ni ya miwani ikifuatiwa na mtoto wa jicho ambayo husababisha upofu.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Vision Care Bw. Taegyun Kim amesema wataendelea kushirikiana na Muhimbili katika kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya.