+255 222215701   info@mloganzila.or.tzMloganzila yaanzisha huduma ya kuweka puto kwenye tumbo la chakula kusaidia wenye uzito mkubwa

Dec 21 2022

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa huduma mpya ya kuweka puto maalumu kwenye tumbo la chakula kwa watu wenye uzito ulipitiliza (intragastic ballon) iliyozinduliwa Mloganzila

Daktari Bingwa wa Upasuaji Mfumo wa Chakula, Dkt. Eric Muhumba akizungumzia namna zoezi hilo lilivyofanyika kwa mafaniko.

Timu ya wataalamu MNH-Mloganzila wakiongozwa na Dkt. Eric Muhumba (wakwanza kulia) wakimuwekea mtu mwenye uzito uliopitiliza puto maalumu litakalomsaidia kupunguza uzito.

 Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili , Naibu Mkurugenzi wa MNH-Mloganzila , Mjumbe wa Kamati ya Utalii Tiba wakiwa katika picha ya pamoja na timu ya wataalamu walishiriki katika zoezi hilo 

Mjumbe wa Kamati ya Utalii Tiba (Medical Tourism) Bw. AbdulMarik Mollel akielezea namna gani huduma hiyo itakavyoweza kufungua milango kwa watu kutoka nchi jirani kuifuata huduma hiyo

 


Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imezindua huduma mpya ya kuweka puto maalumu kwenye tumbo la chakula kwa watu wenye uzito uliopitiliza (intragastic ballon) ambayo itasaidia kupunguza nafasi kwenye tumbo la chakula hivyo kusababisha mtu kula kidogo jambo ambalo litapelekea kupungua uzito.

Akizindua huduma hiyo leo Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema, Mloganzila ndio Hospitali ya kwanza ya umma Tanzania kutoa huduma hiyo hivyo amewapongeza wataalamu kwa kufanikisha jambo hilo" amesema Prof. Janabi

“Hadi leo tumefanya kwa watu 3 na kuna zaidi ya watu 12 ambao wanahitaji huduma hiyo, wanaotakiwa kupatiwa huduma hii ni wale wenye uzito uliopitiliza ambao ni kuanzia kilo 100.

Kuhusu gharama za huduma hiyo, Prof. Janabi amefafanua kwamba kwa Mloganzila inagharimu TZS 3.5 Mil hadi TZS 4 Mil wakati nje ya nchi ni  zaidi ya TZS 15 Mil.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dkt. Eric Muhumba amesema huduma ya kuweka puto hufanyika kwa dakika 20 ambapo hufanyika kwa kutumia mashine ya Endoscopia (Endoscopy Mashine) hivyo haihusishi upasuaji wa aina yoyote.

Dkt. Eric ameongeza kuwa puto likishawekwa tumboni hukaa kwa muda kati ya miezi sita hadi nane ndipo hutolewa na baada ya hapo mtu huyo atakuwa ameshajenga utamaduni wa kula kidogo hivyo atakuwa amepuguza uzito wa kutosha.

Pia Dkt. Eric ameishauri jamii kufanya mazoezi na kula chakula kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa lishe ili kuwa na afya bora na kuepuka kupata uzito uliopitiliza ambao unasababisha magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari, magonjwa ya moyo na kiharusi.

Naye, Mjumbe wa Kamati ya Utalii Tiba (Medical Tourism) Bw. AbdulMarik Mollel ameipongeza MNH-Mloganzila kwa kuzindua huduma hiyo ambayo itafungua milango kwa watu kutoka nchi jirani kuifuata kwa kuwa ni salama na gharama zake ni nafuu hivyo kusaidia kuitangaza Tanzania.