+255 222151367/9   info@mloganzila.or.tzDkt. Gwajima Awataka Wananchi Kutumia Fursa Ya Kupima Macho Banda La Muhimbili

Oct 29 2021

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wananchi waliotembelea banda la Muhimbili kufanyiwa uchunguzi wa macho.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mh. Jabir Shekimweri akielezea namna alivyofurahishwa na huduma inayotolewa na wataalamu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga & Mloganzila katika  Maonyesho ya Karibu Dodoma Festival yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

Wataalamu wa Macho wakiendelea kufanya uchunguzi  kwa wananchi waliotembelea banda la Hospitali ya Taifa MuhimbilI Upanga na Mloganzila.

Baadhi ya wananchi waliofika kwenye banda la Muhimbili wakisubiri kufanyiwa uchunguzi wa macho.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wananchi wa jiji la Dodoma na maeneo jirani kutumia fursa  na kujitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi wa macho katika banda la Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Dkt. Gwajima ametoa kauli hiyo alipotembelea  banda la Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila  katika Maonyesho ya Karibu Dodoma Festival yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

Pia ameipongeza hospitali ya Taifa Muhimbili pamoja na wataalamu kwa kuendesha zoezi la upimaji bure kwa watu wa Dodoma. 

“Nawapongeza sana wataalamu kwa huduma mnayoitoa kwa wananchi wa Dodoma hivyo nawasihi wananchi  kujitokeza kutumia fursa hii  kufanya uchunguzi wa macho katika banda la Hospitali ya Muhimbili kwa kuwa kuna wataalamu wabobezi ” amesema Dkt. Gwajima.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mh. Jabir Shekimweri ameelezea jinsi alivyofurahishwa na upatikanaji wa huduma na kwamba na yeye  ni mnufaika kwa kuwa amepata fursa ya kupima macho na kupatiwa miwani ya kumsaidia kusoma.

Naye Daktari  Bingwa wa Macho kutoka Muhimbili Upanga Dkt. Neema Moshi   amesema kuwa asilimia kubwa ya wagonjwa waliochunguzwa  wamekutwa na matatizo mbalimbali ya ikiwemo  kutokuona mbali, kutokuana karibu, mzio, mtoto wa jicho na presha ya macho.