+255 222151367/9   info@mloganzila.or.tzKOFIH yaendelea kusaidia uboreshaji wa huduma za kibingwa Mloganzila.

Apr 12 2021

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi (katikati) akifafanua jambo wakati alipokutana na wawakilishi kutoka KOFIH kujadili namna watakavyosaidia uboreshaji wa huduma za kibingwa hospitalini hapa.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ufundi wa Hospitali ya Mloganzila, Mhandisi Veilla Matee (wa kwanza kushoto) akiongoza ziara ya kutembelea baadhi ya maeneo ya kutolea huduma.

Mhandisi Veilla Matee akielezea baadhi ya mashine zilizopo hospitalini hapa ambazo hazitumiki kutokana na ukosefu wa baadhi ya vifaa.

Kiongozi wa msafara kutoka KOFIH Bi Gloria Kim akielezea mipango ya kushirikiana kwa kuendesha mafunzo na kutoa msaada wa vifaa tiba vitakavyotumika kutengeneza baadhi mashine ambazo hivi sasa hazitumiki.

Wawakilishi kutoka Taasisi ya Korea Foundation for International Healthcare (KOFIH) leo wametembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila na kujadili namna watakavyoweza kuboresha huduma za kibingwa kwa kutoa msaada wa vifaa tiba na mafunzo kwa wataalamu.

Viongozi hao wametembelea wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), Idara ya Magonjwa ya Dharura na Wodi ya watoto wachanga chini ya siku 28 wanaohitaji uangalizi maalumu (Neonatal Intensive Care Unit).

Mwaka 2019 KOFIH ilitoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya TZS. 331,383,000 Mil ambapo msaada huo ulijumuisha vifaa tiba vya kufanyia upasuaji masikio, pua na koo pamoja na vifaa vya ufundi kwa ajili ya matengenezo ya vifaa tiba.

Pia wamefanikiwa kutoa mafunzo kwa wataalamu wa MNH-Mloganzila kwa njia ya mtandao ya namna ya kutumia baadhi ya vifaa ikiwemo mashine ya kuvunja mawe kwenye figo na mfumo wa mkojo kwa njia ya mawimbi mshituko (Extracorporeal Shock Wave Lithotripsy).