Oct 26 2022
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi akizungumza na Madaktari wa Magonjwa ya Moyo na Madaktari wa Magonjwa wa Mishipa ya Fahamu wakati wa kikao hicho kilichofanyika hospitali hapa (kushoto) ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi.
Madaktari wa Magonjwa ya Moyo na Madaktari wa Magonjwa wa Mishipa ya Fahamu wakimsikiliza Mkurugenzi Mtwendaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema hospitali imeamua kuimarisha kliniki za magonjwa ya moyo na magonjwa mfumo wa fahamu MNH-Mloganzila kuanzia Novemba 1, 2022.
Prof. Janabi ameyasema hayo leo wakati akizungumza na madaktari wa magonjwa ya moyo na madaktari wa magonjwa ya mishipa ya fahamu katika kikao kilichofanyika Mloganzila.
Prof. Janabi amesema uamuzi huo umetokana na Hospitali ya Mloganzila kuwa na vifaa vya kisasa, wataalam na eneo la kutosha kuwezesha kutoa huduma hizo kwa ubora unaotakiwa.
“Hapa Mloganzila kuna vifaa vya kutosha kutoa huduma hizi, hivyo tumefanya uamuzi huu ili kuunganisha nguvu katika kuwahudumia wagonjwa, ni matumaini yangu wananchi watakuwa na mtazamo chanya kwakuwa lengo letu ni kuwapatia huduma bora na kukidhi mahitaji yao” amesema Prof. Janabi.
Prof. Janabi amewaomba madaktari hao kuwahamasisha wagonjwa kuja kupata matibabu ya magonjwa hayo Hospitali ya Mloganzila na kuwahakikishia kuwa ubora wa huduma zinazotolewa ni za viwango vinavyohitajika.
Kwa upande wao madaktari wamempongeza Prof. Janabi kwa ubunifu wa kuanzisha Huduma hizo katika Hospitali ya Mloganzila.
Mkurugenzi Mtendaji ameendelea kukutana na watumishi wa kada mbalimbali kwa lengo la kuweka mikakati na kubadilishana uzoefu wa namna ya kuboresha huduma za matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili.
2.