Muhimbili National Hospital – Mloganzila

MUHIMBILI YAPONGEZWA KWA KUIMARISHA HUDUMA ZA UBINGWA BOBEZI NCHINI.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga na Mloganzila) kuendelea kuimarisha huduma za ubingwa bobezi hapa nchini na kupunguza rufaa za kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu hayo

Mhe. Simbachewene ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la hospitali hiyo, katika maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma inayoadhimishwa kitaifa Viwanja vya Chinangali Park, Mkoani Dodoma.

“Nawapongeza sana, Muhimbili ni hospitali ya kisasa mno, haina tofauti na hospitali za nje ya nchi, ina watumishi wanaojituma sana, mazingira yake ni ya kuvutia, wodi zake ni safi, zina mashuka masafi, endeleeni kuchapa kazi” ameongeza Mhe. Simbachawene.

Mhe. Simbachawene amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika sekta ya afya kitu kilichofanya hospitali hizo kuwa kimbilio kwa watanzania na watu kutoka mataifa ya jirani.

Aidha, Dkt. Simbachawene ameongeza kuwa serikali itaendelea kufanya uwekezaji wa kutosha ili baada ya muda mfupi ujao kusiwe na mtanzania yeyote atakayekwenda nje ya nchi kutafuta huduma hizo kwakuwa zitakuwa zinapatikana hapa hapa nchini.

Katika maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma mwaka 2025, yaliyobeba kauli mbiu “Himiza matumizi ya mifumo ya kidijiti ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji, Hospitali ya Taifa Muhimbili inatoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya macho, magonjwa ya akina mama na afya uzazi, magonjwa ya kisukari na homoni na magonjwa ya dharura na ajali.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top