+255 222151367/9   info@mloganzila.or.tzWanachi zaidi ya 200 wapimwa afya bure Mloganzila

Jan 15 2021

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi akizungumza katika zoezi la upimaji afya bure na kutoa elimu juu ya magonjwa yasiyoambukiza kwa wananchi,kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi Muhimbili -Upanga Sis. Zuhura Mawona ,(kushoto) ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi Muhimbili-Mloganzila

Sis. Redemptha Matindi akielezea sababu zinazochangia magonjwa yasiyo ya kuambukiza na namna jamii inavyoweza kuepuka.

Baadhi ya wananchi wakipata huduma ya kupimwa shinikizo la damu.

Wananchi wakisubiri kupata huduma ya kupima afya bure katika Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila.

Wauguzi Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila wamefanya zoezi la upimaji afya bure kwa wananchi na kutoa elimu juu ya magonjwa yasiyoambukizwa ikiwa ni sehemu ya kuhitimisha mwaka wa wauguzi duniani 2020.

Katika zoezi hilo zaidi ya watu 200 wamepata fursa ya kupima magonjwa kama vile shinikizo la damu,kisukari,uzito pamoja na urefu na kupata elimu juu ya magonjwa yasiyoambukizwa bila malipo .

Akizungumza wakati wa zoezi hilo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema kuwa takwimu za shirika la Afya Duniani mwaka (2018) zinaonesha kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanaelekea kuzidi vifo vitokanavyo na magonjwa yanayoambukiza ambapo kila mwaka watu milioni 41 hufariki na asilimia 71 ya vifo vyote duniani husababishwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

“Wauguzi wamejitolea kutimiza wajibu wao kwa kupima afya bure na kutoa elimu kama zawadi kwa jamii tunayoihudumia ili kufahamu zaidi juu ya magonjwa haya  na namna ya kuweza kuyaepuka kwani  takwimu za Shirika la Afya Duniani mwaka (2018)  zinaonesha  kuwa  magonjwa haya yanaongezeka kwa kasi kubwa na takribani asilimia 33 ya vifo vyote Tanzania vinasababishwa na magonjwa yasiyoambukiza”.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Sis. Redemptha Matindi  amesema kuwa jamii itaweza kuepuka magonjwa haya kwa kubadili mfumo wa maisha kwani magojwa haya husababishwa na  uvutajiwa sigara,kutokufanya mazoezi,matumizi ya vilevi,ulaji wa lishe duni.shinikizo la juu la damu,uzito uliokithiri,kiwango kikubwa cha sukari mwilini na kuwepo kwa lehemu kwenye mishipa ya damu.

“Njia bora ya kupunguza na kuepuka magonjwa hayani kwa kubadili mfumo wa maisha kwa kuanza na mtu binafsi,jamii na taifa kwa ujumla”

Zoezi hili limeanza jana na linataraji kumalizika kesho na  watu wote watakaofanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa na magonjwa haya watapata  fursa ya kumuona daktari bingwa bure.