+255 222215701   info@mloganzila.or.tzMatibabu ya haraka yanaweza kukuepusha na ugonjwa wa tezi dume.

Sep 20 2022

Mfano wa mgonjwa aliyeathirika na ugonjwa wa tezi dume

Jamii imeshauriwa kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara ili kujikinga na kuepuka magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa tezi dume unaoshambulia wanaume hususani wenye umri wa miaka 40 na kuendelea.

Rai hiyo imetolewa na Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mfumo wa Mkojo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mlonganzila Dkt. Hamisi Isaka alipokuwa akifanya mahojiano maalum kuhusu sababu, dalili pamoja na athari za ugonjwa wa tezi dume.

“Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa ugonjwa wa tezi dume unashambulia wanaume wenye umri kuanzia miaka arobaini (40) na kuendelea, hii inatokana na kuongezeeka kwa vichocheo vya homoni katika mwili ambavyo vinasababisha tezi dume kukua na kuathiri kibofu cha mkojo” amesema Dkt.Isaka.

Dkt.Isaka amebainisha dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kukojoa mara kwa mara hususani nyakati za usiku, maumivu makali wakati wa kukojoa, kushindwa kuzuia mkojo, kutumia nguvu nyingi kusukuma mkojo na presha ya mkojo kuwa ndogo.

Dkt. Isaka ameongeza kuwa kwa kawaida mtu anatakiwa kutumia chini ya sekunde 30 kukojoa, endapo mtu ataona anatumia zaidi ya muda huo anatakiwa kufika kituo cha kutolea huduma za afya ili aweze kufanyiwa uchunguzi na hatimaye kupata matibabu.

Akitaja baadhi ya madhara ya ugonjwa huo Dkt. Isaka amesema ni pamoja na kupata maambukizi kwenye njia ya mfumo wa mkojo (UTI), figo kushindwa kufanya kazi, kutengeneza mawe kwenye kibofu cha mkojo au figo wakati mwingine kushindwa kupata mkojo kabisa.

Akizungumzia matibabu ya ugonjwa huo Dkt. Isaka amesema inategemea na ukubwa wa tatizo ambapo katika hatua za awali mgonjwa anaweza kutumia dawa na tatizo kupona kupona kabisa.

Aidha, kama Mgonjwa atachelewa kupata matibabu katika hatua za awali atalazimika kufanyiwa upasuaji wa kawaida na kutoa tezi au kufanya upasuaji kwa kutumia vifaa maalum (minially invasive procedure).

Dkt. Isaka pia ameitaka jamii kutumia dawa kwa usahihi, kufuata maelekezo ya daktari ambapo itamfanya arejee katika hali ya kwaida na kuendelea na shughuli zake baada ya wiki sita hadi nane.

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila inatoa huduma za uchunguzi na matibabu ya tezi dume, kwa ushauri zaidi fika hospitalini katika kliniki ya Magonjwa ya Mfumo wa Mkojo kila siku ya Jumanne na Alhamisi kuanzia saa 2:00 Asubuhi-9:00 Alasiri, Ghorofa ya kwanza.